Wafilipi 4:1-7
Wafilipi 4:1-7 NENO
Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji langu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana Isa, ninyi wapendwa wangu. Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana Isa. Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana Isa siku zote, tena nasema furahini! Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana Isa yu karibu. Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Al-Masihi Isa.