Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 28

28
Sadaka za kila siku
(Kutoka 29:38-46)
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Wape Waisraeli agizo hili, uwaambie: ‘Hakikisheni kwamba mnaniletea mimi kwa wakati uliowekwa chakula kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, kama harufu nzuri ya kupendeza.’ 3Waambie: ‘Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto mnayomtolea Mwenyezi Mungu: wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na dosari, kuwa sadaka ya kawaida ya kuteketezwa kila siku. 4Andaa mwana-kondoo mmoja asubuhi na mwingine jioni, 5kila mmoja atolewe pamoja na sadaka ya nafaka sehemu ya kumi ya efa#28:5 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja. ya unga laini uliochanganywa pamoja na robo ya hini#28:5 Robo ya hini ni sawa na lita moja. ya mafuta ya zeituni. 6Hii ni sadaka ya kawaida ya kuteketezwa iliyoanzishwa katika Mlima Sinai kama harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. 7Sadaka ya kinywaji itakayotolewa pamoja na kila mwana-kondoo ni robo ya hini ya kinywaji kilichochachuka. Mimina sadaka ya kinywaji kwa Mwenyezi Mungu mahali patakatifu. 8Andaa yule mwana-kondoo wa pili jioni, pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kama ulivyofanya kwa ile sadaka nyingine ya asubuhi. Hii ni sadaka iliyotolewa kwa kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Sadaka za Sabato
9“ ‘Siku ya Sabato, utatoa sadaka ya wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari pamoja na sadaka yake ya kinywaji na sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu mbili za kumi ya efa#28:9 Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo 2. ya unga laini uliochanganywa na mafuta. 10Hii ni sadaka ya kuteketezwa itakayotolewa kwa ajili ya kila Sabato, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya kinywaji.
Sadaka za kila mwezi
11“ ‘Siku ya kwanza ya kila mwezi, mtamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa ya fahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasiokuwa na dosari. 12Pamoja na kila fahali, kutakuwa na sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa#28:12 Sehemu tatu za kumi ya efa ni sawa na kilo 3., uliochanganywa na mafuta, pamoja na kondoo dume mmoja, sadaka ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; 13pamoja na kila mwana-kondoo, sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Hii ni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri, sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. 14Pamoja na kila fahali kutakuwa na sadaka ya kinywaji nusu ya hini#28:14 Nusu ya hini ni sawa na lita 2. ya divai; pamoja na kila kondoo dume, theluthi moja ya hini#28:14 Theluthi moja ya hini ni sawa na lita 1.2.; na pamoja na kila mwana-kondoo, robo hini. Hii ni sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi itakayotolewa kila mwandamo wa mwezi kwa mwaka. 15Zaidi ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya kinywaji, mbuzi mmoja dume atatolewa kwa Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya dhambi.
Pasaka
(Walawi 23:5-14)
16“ ‘Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, itafanyika Pasaka ya Mwenyezi Mungu. 17Katika siku ya kumi na tano ya mwezi huo itakuwa sikukuu; kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. 18Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, msifanye kazi za kawaida. 19Leteni mbele za Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo dume saba wenye umri wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari. 20Pamoja na kila fahali, andaa sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi ya efa; 21pia pamoja na kila mmoja wa wale wana-kondoo saba, andaa sehemu ya kumi ya efa. 22Pia mtoe beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi ambaye atafanya upatanisho kwa ajili yenu. 23Andaa hizi licha ya zile sadaka za kawaida za kuteketezwa za kila asubuhi. 24Kwa njia hii andaa chakula cha sadaka ya kuteketezwa kila siku, kwa siku saba kama harufu nzuri impendezayo Mwenyezi Mungu. Hii itaandaliwa licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji. 25Siku ya saba mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.
Sikukuu ya Majuma
(Walawi 23:15-22)
26“ ‘Siku ya malimbuko, mnapomletea Mwenyezi Mungu sadaka ya nafaka mpya wakati wa Sikukuu ya Majuma, mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida. 27Mlete sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja, na pia wana-kondoo saba wenye umri wa mwaka mmoja, kama harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. 28Pamoja na kila fahali itatolewa sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini; 29na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa kila mmoja wa wana-kondoo saba. 30Ongeza beberu mmoja kwa kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 31Andaa hizi sadaka pamoja na sadaka zake za vinywaji, kuwa nyongeza ya sadaka za kawaida za kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka. Hakikisha kuwa wanyama hao hawana dosari.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 28: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia