Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Nehemia 2:1-8

Nehemia 2:1-8 NEN

Katika mwezi wa Nisani mwaka wa ishirini wa utawala wa Mfalme Artashasta, wakati divai ilipoletwa kwake, niliichukua na kumpa mfalme. Sikuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele yake kabla ya hapo. Basi mfalme akaniuliza, “Kwa nini uso wako unaonekana una huzuni wakati wewe si mgonjwa? Jambo hili si kitu kingine bali ni huzuni ya moyo.” Niliogopa sana, lakini nikamwambia mfalme, “Mfalme na aishi milele! Kwa nini uso wangu usiwe na huzuni wakati mji walipozikwa baba zangu umebaki magofu, na malango yake yameteketezwa kwa moto?” Mfalme akaniambia, “Je, haja yako ni gani?” Ndipo nikaomba kwa Mungu wa mbinguni, na nikamjibu mfalme, “Kama ikimpendeza mfalme, na kama mtumishi wako amepata kibali machoni pake, anitume kule mji wa Yuda, mahali baba zangu walipozikwa, ili niweze kuujenga upya.” Kisha mfalme, na malkia akiwa ameketi karibu naye, akaniuliza, “Safari yako itachukua muda gani, nawe utarudi lini?” Ilimpendeza mfalme kunituma, kwa hiyo nikapanga muda. Pia nikamwambia, “Kama ikimpendeza mfalme, naomba nipewe barua kwa watawala wa Ngʼambo ya Frati, ili wanipe ulinzi mpaka nifike Yuda. Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, na ukuta wa mji, na makao yangu nitakapoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu.