Marko 3:7-19
Marko 3:7-19 NENO
Yesu na wanafunzi wake wakaondoka huko, wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya wakamfuata. Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, makundi ya watu wakamjia kutoka Yudea, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa maeneo ya Tiro na Sidoni. Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake watayarishe mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” Lakini aliwaonya wasiwaambie wengine kumhusu. Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. Akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa naye, na awatume kwenda kuhubiri na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu. Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro); Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo); Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.