Marko 15:42-47
Marko 15:42-47 NEN
Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi, yaani siku moja kabla ya Sabato, Yosefu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu. Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa. Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.