Marko 11:12-23
Marko 11:12-23 NEN
Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo. Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake. Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji. Asubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!” Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa.