Mathayo 8:14-22
Mathayo 8:14-22 NEN
Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na alichukua magonjwa yetu.” Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ngʼambo ya ziwa. Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.” Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”