Mathayo 6:24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33
Mathayo 6:24 NENO
“Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.
Mathayo 6:25 NENO
“Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?
Mathayo 6:26 NENO
Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani kuliko hao ndege?
Mathayo 6:27 NENO
Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
Mathayo 6:28 NENO
“Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi.
Mathayo 6:29 NENO
Lakini nawaambia, hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.
Mathayo 6:30 NENO
Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba?
Mathayo 6:31 NENO
Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’
Mathayo 6:32 NENO
Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote.
Mathayo 6:33 NENO
Lakini utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.