Mathayo 23:1-22
Mathayo 23:1-22 NENO
Kisha Isa akaambia wale umati wa watu na wanafunzi wake: “Walimu wa Torati na Mafarisayo wameketi kwenye kiti cha Musa, hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza. “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao. Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi. Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Mwalimu.’ “Lakini ninyi msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Al-Masihi. Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa. “Lakini ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [ Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.] “Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa Jehanamu mara mbili kuliko ninyi! “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’ Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’ Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu? Basi, mtu anayeapa kwa madhabahu, anaapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake. Naye mtu anayeapa kwa Hekalu, anaapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake. Naye anayeapa kwa mbingu, anaapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye anayeketi kwenye kiti hicho.