Mathayo 15:29-38
Mathayo 15:29-38 NENO
Isa akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. Umati mkubwa wa watu wakamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli. Kisha Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga watu wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kulisha umati mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?” Isa akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.” Isa akaagiza watu wote waketi chini. Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akamshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Idadi ya watu walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.