Mathayo 12:38-45
Mathayo 12:38-45 NEN
Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.” Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.” “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”