Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 7:36-50

Luka 7:36-50 NEN

Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani. Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato. Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.” Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.” Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.” “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500 na mwingine dinari hamsini. Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?” Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.” Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake. Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.” Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?” Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Luka 7:36-50