Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 7:31-50

Luka 7:31-50 NENO

Isa akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini? Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema: “ ‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliwaimbia nyimbo za maombolezo, lakini hamkulia.’ Kwa maana Yahya alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.” Basi Farisayo mmoja alimwalika Isa kwake ale chakula. Hivyo Isa akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kuketi mezani. Palikuwa na mwanamke mmoja katika mji ule aliyekuwa mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Isa alikuwa akila chakula nyumbani mwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Isa akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato. Yule Farisayo aliyemwalika Isa alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.” Isa akamjibu, “Simoni, nina jambo la kukuambia.” Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.” “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari mia tano na mwingine dinari hamsini. Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda zaidi yule aliyewasamehe?” Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Isa akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.” Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake. Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.” Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?” Isa akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”