Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 4:16-31

Luka 4:16-31 NEN

Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.” Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.” Wote waliokuwako wakamsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?” Yesu akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ” Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe. Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Eliya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima. Hata hivyo Eliya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Elisha, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.” Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima mahali ambapo mji huo ulikuwa umejengwa, ili wamtupe chini kutoka kwenye mteremko mkali. Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya huo umati wa watu akaenda zake. Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.