Luka 4:1-30
Luka 4:1-30 NENO
Isa, akiwa amejaa Roho Mtakatifu wa Mungu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho wa Mungu hadi nyikani, ambako alijaribiwa na ibilisi kwa siku arobaini. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa. Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’” Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonesha milki zote za dunia kwa mara moja. Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. Hivyo ukinisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.” Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’” Kisha ibilisi akampeleka hadi Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, kwa maana imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika wake ili wakulinde kwa uangalifu; nao watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’” Isa akamjibu, “Imenenwa: ‘Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.’” Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Isa hadi wakati mwingine ufaao. Kisha Isa akarudi hadi Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho wa Mungu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando. Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu. Isa akaenda Nasiri, alipolelewa, na siku ya Sabato alienda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu amenipaka mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoteswa, na kutangaza mwaka wa Mwenyezi Mungu uliokubalika.” Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.” Watu wote walimsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yusufu?” Isa akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ” Isa akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe. Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Ilya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima. Hata hivyo Ilya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Al-Yasa, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.” Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima ambao mji huo ulikuwa umejengwa juu yake, ili wamtupe chini kutoka mteremko mkali. Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya umati huo wa watu akaenda zake.