Luka 1:39-56
Luka 1:39-56 NEN
Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi. Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti. Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.” Naye Maria akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu, kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa, kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu. Rehema zake huwaendea wale wamchao, kutoka kizazi hadi kizazi. Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao. Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi, lakini amewainua wanyenyekevu. Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu. Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.” Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.