Yoshua 18:1-9
Yoshua 18:1-9 NEN
Kusanyiko lote la Waisraeli likakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao. Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Chagueni watu watatu kutoka kwenye kila kabila. Nitawatuma hao watu kukagua hiyo nchi na kuniandikia mapendekezo ya mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Nao watanirudia. Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yosefu katika nchi yake upande wa kaskazini. Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura kwa kura mbele za BWANA Mungu wetu. Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa BWANA ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Mose mtumishi wa BWANA aliwapa.” Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuandika vizuri kuhusu hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo kuihusu. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za BWANA.” Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo.