Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 9:18-33

Yohana 9:18-33 NENO

Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu akapata kuona, hadi walipowaita wazazi wake. Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. Lakini hatujui jinsi anavyoweza kuona sasa, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni; yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi, kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Isa kuwa ndiye Al-Masihi atafukuzwa kutoka sinagogi. Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.” Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.” Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.” Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?” Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?” Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake! Sisi ni wanafunzi wa Musa. Tunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini mtu huyu hatujui anakotoka.” Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu! Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii. Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu. Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”