Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 7:10-24

Yohana 7:10-24 NEN

Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri. Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?” Kulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?” Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?” Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 7:10-24