Yohana 6:41-59
Yohana 6:41-59 NENO
Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Huyu si Isa, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?” Hivyo Isa akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. Mimi ni mkate wa uzima. Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. Lakini hapa kuna mkate kutoka mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?” Hivyo Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.