Yohana 6:15-25
Yohana 6:15-25 NENO
Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake. Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wameenda mwendo wa maili tatu au nne, walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda. Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo waliona kwamba palikuwa na mashua moja tu, na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana Isa kumshukuru Mungu. Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwa hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa. Walipomkuta Isa ng’ambo ya bahari wakamuuliza, “Mwalimu, umefika lini huku?”