Yohana 6:1-21
Yohana 6:1-21 NENO
Baada ya haya, Isa alienda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya (ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia). Umati mkubwa wa watu waliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. Kisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Isa alipotazama na kuona umati ule mkubwa wa watu wakimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya. Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa watu hawa wote?” Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi (palikuwa na wanaume wapatao elfu tano). Ndipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula. Baada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake. Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wameenda mwendo wa maili tatu au nne, walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.