Yohana 5:30-47
Yohana 5:30-47 NEN
“Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli. “Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli. Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa. Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake. “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye alinituma. Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima. “Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu. Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu? “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu. Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu. Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”