Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19:31-42

Yohana 19:31-42 NENO

Ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, na siku iliyofuata ingekuwa Sabato maalum. Kwa kuwa viongozi wa Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe, na miili iondolewe kwenye misalaba. Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Yesu, na ya yule mwingine pia. Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake. Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni, na mara pakatoka damu na maji. Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini. Kwa maana mambo haya yalitukia ili andiko litimie, lisemalo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” Tena andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.” Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Yesu, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Yesu. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua. Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Yesu usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini. Wakauchukua mwili wa Yesu, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi. Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado. Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Yesu humo.