Yohana 19:16-30
Yohana 19:16-30 NENO
Ndipo Pilato akamkabidhi Isa kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Isa. Isa, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wawili, mmoja kila upande wake, naye Isa katikati. Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Isa; likasema: ISA AL-NASIRI MFALME WA WAYAHUDI. Kwa kuwa mahali hapo Isa aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.” Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!” Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini. Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari. Karibu na msalaba wa Isa walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Mariamu mke wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Isa alipomwona mama yake mahali pale, na yule mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama karibu, Isa akamwambia mama yake, “Mama, huyu hapa ndiye mwanao.” Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyu hapa ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Isa nyumbani mwake. Baada ya haya, akijua kuwa mambo yote yamemalizika, na ili kutimiza Maandiko, Isa akasema, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. Baada ya kuionja hiyo siki, Isa akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.