Yohana 13:18-30
Yohana 13:18-30 NEN
“Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili Andiko lipate kutimia, kwamba, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’ “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.” Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi wake ambaye Yesu alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.” Yule mwanafunzi akamwegemea Yesu, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?” Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.” Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini chochote. Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.