Yohana 12:37-50
Yohana 12:37-50 NEN
Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.” Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake. Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu. Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani. “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”