Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 12:1-11

Yohana 12:1-11 NENO

Siku sita kabla ya Pasaka, Isa alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu. Wakaandaa karamu kwa heshima ya Isa. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Isa. Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Isa na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato. Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Isa, ambaye baadaye angemsaliti Isa, akasema, “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini?” Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha. Isa akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.” Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Isa alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Isa, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Isa alikuwa amemfufua. Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia, kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Isa na kumwamini.