Yohana 11:28-46
Yohana 11:28-46 NENO
Baada ya kusema haya, Martha alienda akamwita Mariamu dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.” Mariamu aliposikia hivyo, akaondoka upesi, akaenda hadi alipokuwa Isa. Isa alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha. Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Mariamu nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani kwamba alikuwa anaenda kule kaburini kulilia huko. Mariamu alipofika mahali pale Isa alipokuwa, alipiga magoti miguuni pake na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa.” Isa alipomwona Mariamu akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Isa alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. Akauliza, “Mmemweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.” Isa akalia machozi. Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!” Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?” Isa akafika penye kaburi akiwa amefadhaika sana kwa mara nyingine. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe liliwekwa kwenye ingilio lake. Isa akasema, “Liondoeni jiwe.” Martha dada yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.” Isa akamwambia, “Sikukuambia kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?” Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Isa akainua macho yake juu, akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya watu hawa waliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.” Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti yake, akaita, “Lazaro, njoo huku!” Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Isa akawaambia, “Mfungueni; mwacheni aende zake.” Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Mariamu walipoona yale Isa aliyoyatenda, wakamwamini. Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Isa aliyoyafanya.