Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 11:1-16

Yohana 11:1-16 NENO

Basi mtu mmoja, jina lake Lazaro, alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania, kijiji cha Mariamu na Martha dada yake. (Huyu Mariamu, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye alimpaka Bwana Isa mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.) Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Isa kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.” Lakini Isa aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti, bali ni wa kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Isa aliwapenda Martha, Mariamu na Lazaro ndugu yao. Hata hivyo, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, alikawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi. Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Yudea.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Mwalimu, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?” Isa akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wanaotembea mchana hawawezi kujikwaa, kwa maana wanaona kwa nuru ya ulimwengu huu. Lakini wale wanaotembea usiku hujikwaa kwa sababu hawana nuru ndani yao.” Baada ya kusema haya, Isa akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.” Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” Hata hivyo, Isa alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu. Kwa hiyo Isa akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwako huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.” Tomaso (aliyeitwa Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”