Isaya 8:9-22
Isaya 8:9-22 NEN
Inueni kilio cha vita, enyi mataifa, na mkavunjwevunjwe! Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali. Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa; fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa, kwa maana Mungu yu pamoja nasi. BWANA alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema: “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina, usiogope kile wanachokiogopa, wala usikihofu. BWANA Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu, naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu, atakuwa mtego na tanzi. Wengi wao watajikwaa; wataanguka na kuvunjika, watategwa na kunaswa.” Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria miongoni mwa wanafunzi wangu. Nitamngojea BWANA, ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake. Nitaliweka tumaini langu kwake. Niko hapa, pamoja na watoto ambao BWANA amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni. Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko. Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao. Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.