Isaya 40:12-31
Isaya 40:12-31 NEN
Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani? Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya BWANA, au kumfundisha akiwa kama mshauri wake? Ni nani ambaye BWANA ametaka shauri kwake ili kumwelimisha, naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa? Ni nani aliyemfundisha maarifa au kumwonyesha mapito ya ufahamu? Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo, ni kama vumbi jembamba juu ya mizani, huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini. Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa. Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu, yanaonekana yasio na thamani na zaidi ya bure kabisa. Basi, utamlinganisha Mungu na nani? Utamlinganisha na kitu gani? Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu, naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu na kuitengenezea mikufu ya fedha. Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii huuchagua mti usiooza. Humtafuta fundi stadi wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika. Je, hujui? Je, hujasikia? Je, hujaambiwa tangu mwanzo? Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia? Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia, nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi. Huzitandaza mbingu kama chandarua, na kuzitandaza kama hema la kuishi. Huwafanya wakuu kuwa si kitu, na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure. Mara baada ya kupandwa, mara baada ya kutiwa ardhini, mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini, ndipo huwapulizia nao wakanyauka, nao upepo wa kisulisuli huwapeperusha kama makapi. “Utanilinganisha mimi na nani? Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu mtazame mbinguni: Ni nani aliyeumba hivi vyote? Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine na kuziita kila moja kwa jina lake. Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu, hakuna hata mojawapo inayokosekana. Kwa nini unasema, ee Yakobo, nanyi ee Israeli, kulalamika, “Njia yangu imefichwa BWANA asiione, Mungu wangu hajali shauri langu?” Je wewe, hufahamu? Je wewe, hujasikia? BWANA ni Mungu wa milele, Muumba wa miisho ya dunia. Hatachoka wala kulegea, wala hakuna hata mmoja awezaye kuupima ufahamu wake. Huwapa nguvu waliolegea na huongeza nguvu za wadhaifu. Hata vijana huchoka na kulegea, nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka, bali wale wamtumainio BWANA atafanya upya nguvu zao. Watapaa juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio wala hawatachoka, watatembea kwa miguu wala hawatazimia.