Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 11:7-28

Waebrania 11:7-28 NEN

Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani. Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika. Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao. Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu. Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaki,” Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu. Na kwa kusema kwa mfano, alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu. Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake. Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake. Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waebrania 11:7-28