Waebrania 1:5-14
Waebrania 1:5-14 NEN
Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa?” Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu?” Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.” Anenapo kuhusu malaika asema, “Huwafanya malaika wake kuwa pepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.” Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako. Umependa haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako kwa kukupaka mafuta ya furaha.” Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu; zote zitachakaa kama vazi. Utazikungʼutakungʼuta kama joho, nazo zitachakaa kama vazi. Lakini wewe hubadiliki, nayo miaka yako haikomi kamwe.” Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako”? Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?