Hagai 1
1
Wito wa kujenga Hekalu
1Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la Mwenyezi Mungu lilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na kwa Yoshua#1:1 kwa Kiebrania ni Yeshua, maana yake Yehova ni wokovu mwana wa kuhani mkuu Yehosadaki:
2Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya Mwenyezi Mungu.’ ”
3Kisha neno la Mwenyezi Mungu likaja kupitia kwa nabii Hagai: 4“Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki gofu?”
5Sasa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Zitafakarini vyema njia zenu. 6Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”
7Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Zitafakarini vyema njia zenu. 8Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asema Mwenyezi Mungu. 9“Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe. 10Kwa hiyo, mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake kwa sababu yenu. 11Niliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ng’ombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”
12Kisha Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yoshua kuhani mkuu mwana wa Yehosadaki, pamoja na mabaki yote ya watu wakaitii sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, pamoja na ujumbe wa nabii Hagai, kwa sababu alikuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Watu walimwogopa Mwenyezi Mungu.
13Kisha Hagai, mjumbe wa Mwenyezi Mungu, akawapa watu ujumbe huu wa Mwenyezi Mungu: “Mimi niko pamoja nanyi,” asema Mwenyezi Mungu. 14Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akachochea roho ya Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na roho za mabaki yote ya watu. Walikuja, wakaanza kufanya kazi katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wao, 15siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario.
Iliyochaguliwa sasa
Hagai 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.