Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 8:1-14

Mwanzo 8:1-14 NENO

Mungu akamkumbuka Nuhu na wanyama pori na mifugo wote waliokuwa naye ndani ya safina; akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakapungua. Chemchemi za vilindi zikawa zimefungwa, na malango ya mafuriko ya mbinguni pia yakawa yamefungwa; nayo mvua ikawa imekoma kunyesha. Maji yakaendelea kupungua taratibu katika dunia. Mwishoni mwa siku ya mia moja na hamsini, maji yakawa yamepungua. Na katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu. Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. Kufikia siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili, dunia ilikuwa imekauka kabisa.