Mwanzo 48:1-16
Mwanzo 48:1-16 NEN
Baada ya muda Yosefu akaambiwa kwamba, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu, pamoja naye. Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yosefu amekujia kukuona,” Israeli akakusanya nguvu zake, akaketi kitandani. Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani, huko akanibariki, naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na kuongezeka hesabu yako, nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele wewe na wazao wako baada yako.’ “Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu). Wakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?” Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.” Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.” Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia. Israeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.” Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. Yosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza. Ndipo akambariki Yosefu akisema, “Mungu ambaye baba zangu Abrahamu na Isaki walimtii, Mungu ambaye amekuwa mchungaji wa maisha yangu yote mpaka leo hii, Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote, yeye na awabariki vijana hawa. Na waitwe kwa jina langu na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki, wao na waongezeke kwa wingi katika dunia.”