Mwanzo 44:18-34
Mwanzo 44:18-34 NENO
Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe. Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’ Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’ “Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’ Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’ Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’ Tuliporudi kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema. “Ndipo baba yetu alisema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’ Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutaenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’ “Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili. Mmoja alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo. Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’ “Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu, akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sitamrudisha kwako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’ “Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi wako abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake. Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”