Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:46-57

Mwanzo 41:46-57 NEN

Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. Katika ile miaka saba ya neema nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. Yosefu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya neema nchini Misri, akakihifadhi katika ghala za miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. Yosefu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari, ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi sana kupita kipimo. Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alikuwa amemzalia Yosefu wana wawili wa kiume. Yosefu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” Mwana wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.” Ile miaka saba ya neema huko Misri ikaisha, nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yosefu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. Wakati nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao alipowaagiza Wamisri wote, akisema, “Nendeni kwa Yosefu, nanyi mfanye anachowaambia.” Wakati njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yosefu akafungua ghala za vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.