Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:1-13

Mwanzo 41:1-13 NEN

Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto: Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili, wakati ngʼombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete. Baada yao ngʼombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea mtoni Naili wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. Wale ngʼombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka. Farao akaingia usingizini tena akaota ndoto ya pili: Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyonyaushwa na upepo wa mashariki. Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, kumbe ilikuwa ndoto. Asubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria. Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake. Nayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.”