Mwanzo 4:1-15
Mwanzo 4:1-15 NEN
Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa BWANA nimemzaa mwanaume.” Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake. Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa BWANA. Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. BWANA akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. Kisha BWANA akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua. Kisha BWANA akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” BWANA akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.” Kaini akamwambia BWANA, “Adhabu yangu ni zaidi ya niwezavyo kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga asiyetulia duniani na yeyote anionaye ataniua.” Lakini BWANA akamwambia, “La sivyo, ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba zaidi.” Kisha BWANA akamwekea Kaini alama ili mtu yeyote ambaye angemwona asimuue.