Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 3:14-24

Mwanzo 3:14-24 NENO

Hivyo Bwana Mwenyezi Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko mifugo wote na wanyama pori wote! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako. Nami nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, na kati ya uzao wako na wake; yeye atakuponda kichwa, nawe utamuuma kisigino.” Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana uchungu wakati wa kuzaa kwako; kwa uchungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Akamwambia Adamu, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’ “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako; kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo siku zote za maisha yako. Itakuzalia miiba na mibaruti, nawe utakula mimea ya shambani. Kwa jasho la uso wako utakula chakula chako hadi utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo; wewe u mavumbi na mavumbini utarudi.” Adamu akamwita mkewe jina Hawa, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai. Bwana Mwenyezi Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Kisha Bwana Mwenyezi Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” Hivyo Bwana Mwenyezi Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki mwa Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika kila upande kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.