Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 24:48-67

Mwanzo 24:48-67 NEN

nikasujudu na nikamwabudu BWANA. Nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake. Ikiwa mtaonyesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie, la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.” Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa BWANA, hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema. Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na BWANA alivyoongoza.” Ikawa huyo mtumishi wa Abrahamu aliposikia waliyosema, alisujudu mpaka nchi mbele za BWANA. Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha pamoja na mavazi, akampa Rebeka, pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye. Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale. Walipoamka asubuhi, yule mtumishi, akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.” Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.” Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa BWANA amefanikisha safari yangu, nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.” Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.” Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Akasema, “Nitakwenda.” Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Wakambariki Rebeka, wakamwambia, “Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu, mara elfu nyingi, nao wazao wako wamiliki malango ya adui zao.” Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia zao wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka akaondoka. Basi Isaki alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa anaishi nchi ya Negebu. Isaki akatoka kwenda shambani kutafakari wakati wa jioni, alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja. Rebeka pia akainua macho akamwona Isaki. Akashuka kutoka kwenye ngamia wake na akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule aliye kule shambani anayekuja kutulaki?” Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika. Kisha yule mtumishi akamweleza Isaki mambo yote aliyoyatenda. Ndipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 24:48-67