Mwanzo 19:12-29
Mwanzo 19:12-29 NEN
Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine yeyote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa BWANA dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.” Kwa hiyo Loti alitoka ili kuzungumza na wakwe zake, waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa BWANA yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania. Kunako mapambazuko, malaika wakamhimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.” Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa BWANA alikuwa na huruma kwao. Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!” Lakini Loti akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa. Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.” Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.) Wakati Loti alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. Ndipo BWANA akanyesha moto wa kiberiti uliotoka mbinguni kwa BWANA juu ya Sodoma na Gomora. Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote waliokuwa wanaishi katika miji, hata pia mimea yote katika nchi. Lakini mke wa Loti akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi. Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Abrahamu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za BWANA. Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka kwenye nchi, kama moshi utokao kwenye tanuru. Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare alimkumbuka Abrahamu, akamtoa Loti kutoka kwenye lile janga lililoharibu miji ile ambamo Loti alikuwa ameishi.