Ezekieli 1:1-14
Ezekieli 1:1-14 NENO
Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa miongoni mwa waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu. Katika siku ya tano ya mwezi, mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehoyakini, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yake. Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyong’aa ndani ya moto. Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu, lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea. Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa hao wanne alikuwa na uso wa mwanadamu, na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, na kwa upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng’ombe; pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliokunjuliwa kuelekea juu; kila bawa liligusa bawa la mwenzake kila upande; kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipoenda, walienda pasipo kugeuka. Kuonekana kwa wale viumbe hai kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya wale viumbe; ulikuwa na mwangaza mkali na katika ule moto kulitoka miali ya radi. Wale viumbe walipiga mbio kwenda na kurudi, kama miali ya radi.