Waefeso 1:1-15
Waefeso 1:1-15 NENO
Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mungu. Kwa watakatifu walio Efeso, walio waaminifu katika Al-Masihi Isa. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi. Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Al-Masihi. Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kupitia kwa Isa Al-Masihi kwa furaha na mapenzi yake. Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. Ndani yake tunao ukombozi kupitia kwa damu yake, yaani msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Al-Masihi, ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Al-Masihi. Katika Al-Masihi sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, ili, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Al-Masihi, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. Ninyi pia mliingia ndani ya Al-Masihi mliposikia neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Baada ya kuamini, mlitiwa muhuri ndani yake, huyo Roho Mtakatifu wa Mungu mliyeahidiwa, yeye ambaye ni amana yetu ya kutuhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu, kwa sifa ya utukufu wake. Kwa sababu hii, tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Isa na upendo wenu kwa watakatifu wote