Kumbukumbu 32:44-52
Kumbukumbu 32:44-52 NENO
Musa na Yoshua mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia. Musa alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote, akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii. Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.” Siku hiyo hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Kwea katika safu za Abarimu hadi kilima cha Nebo kilicho Moabu, ng’ambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe. Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Haruni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake. Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli. Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”