Matendo 27:13-26
Matendo 27:13-26 NENO
Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakang’oa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete. Lakini baada ya muda mfupi, ikavuma tufani kubwa iitwayo Eurakilo kutoka kisiwa cha Krete. Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea. Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu. Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo. Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu, kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka kwenye meli. Siku ya tatu, wakatupa vyombo vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe. Wakati jua wala nyota hazikuonekana kwa siku nyingi, na dhoruba iliendelea kuvuma, hatimaye tulikata tamaa ya kuokolewa. Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama mbele yao na kusema: “Enyi watu, kama mngekubali ushauri wangu wa kutosafiri kwa meli kutoka Krete, basi mngejiepusha na uharibifu na hasara hii. Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia. Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ninayemwabudu alisimama karibu nami, akaniambia, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe.’ Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia. Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”