Matendo 23:23-35
Matendo 23:23-35 NENO
Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari mia mbili, wapanda farasi sabini, na watu mia mbili wenye mikuki. Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.” Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo: Klaudio Lisia. Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi. Salamu. Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi. Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya Baraza la Wayahudi. Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo. Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na njama dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako. Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta hadi Antipatri. Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari. Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake. Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia, alisema, “Nitasikiliza kesi yako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.