Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 20:1-16

Matendo 20:1-16 NEN

Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Alipokuwa anakaribia kuanza safari kwa njia ya bahari kwenda Shamu, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yake, aliamua kurudi kupitia njia ya Makedonia. Paulo alikuwa amefuatana na Sopatro mwana wa Piro, Mberoya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike na Gayo, mtu wa Derbe, Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka sehemu ya Asia. Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. Lakini sisi tukasafiri kwa njia ya bahari kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba. Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane. Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana. Tukatangulia melini tukasafiri mpaka Aso ambako tungempakia Paulo. Alikuwa amepanga hivyo kwa maana alitaka kufika kwa miguu. Alipotukuta huko Aso, tulimpakia melini, tukasafiri wote mpaka Mitilene. Kutoka huko tuliendelea kwa njia ya bahari, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko sehemu za Asia, kwa sababu alikuwa anatamani kama ikiwezekana kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 20:1-16